Usomaji shahada za juu unavyogeuka shubiri vyuoni

Muktasari:

Wakati mjadala uliopo sasa ukiwa kwa nini watu wengi wanapendelea kuitwa wasomi wa PhD, mengine yamebainika kuhusu taratibu za usomaji wa shahada za juu katika baadhi ya vyuo vikuu nchini.

By Abeid Poyo, Mwananchi [email protected]

Wakati mjadala uliopo sasa ukiwa kwa nini watu wengi wanapendelea kuitwa wasomi wa PhD, mengine yamebainika kuhusu taratibu za usomaji wa shahada za juu katika baadhi ya vyuo vikuu nchini.

Kuna madai ya kuwapo kwa ukiritimba kutoka kwa wasimamizi, wanaodaiwa kufikia hatua ya kuwafelisha wanafunzi, au kuwawekea vikwazo vinavyowafanya waishie njiani.

Mifumo na taratibu za kielimu vyuo vikuu inaelekeza wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamifu (PhD), wanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa wahadhiri wa ndani.


Waliopitia machungu

Hata hivyo, kwa baadhi ya wanafunzi, wasimamizi hawa wamegeuka kuwa shubiri kwao. Wapo ambao hawatamani kurudi masomoni kama ilivyo kwa Adam Yasin, anayesema elimu imemtumbukia nyongo kutokana na masaibu aliyokutana nayo kutoka kwa msimamizi wake.

Yasin aliomba udahili wa kusomea shahada ya uzamili katika chuo kikuu kimoja kikongwe nchini.

Pamoja na kufaulu tamrini (course work) kwa kupata GPA ya alama 4.5, mwanafunzi huyo alikwama katika hatua ya utafiti kwa kile anachodai kuwa ni ukiritimba na husuda kutoka msimamizi wake.

Akizungumza na Mwananchi, Yasin anasimulia: “Sababu kubwa ni kwamba wengi (wasimamizi) wana ukiritimba uliogubikwa na husda ukipambwa na ukabila na kujuana. Sasa ikiwa kuna tofauti ya ukabila na huna nafasi nzuri ya kujulikana ukitegemea tu akili yako, humalizi. Mimi nilipata GPA ya 4.5 kwenye course work (tamrini) lakini nikaishia kwenye utafiti.

“But it was a disaster, I am telling you. (Ni balaa nakwambia). Kuna wakati alikuwa akisha kunywa pombe. Amelewa ndiyo alikuwa anafunguka akisema, nikusimamie mimi umalize masters (shahada ya uzamili) yako, thubutu...kwanza sijawahi kusimamia mwanamume mimi. Wewe ndio wa kwanza. Nimesimamia kina…. (anataja majina ya wanafunzi wanawake na wote kutoka kabila lake). Wewe sijui umetokea wapi aisee.”

Yasin anasema utafiti wake japo ulikuwa umefadhiliwa, msimamizi wake bado hakuwa tayari kumpatia fedha kwa ajili ya kufanya majaribio ya sampuli karibu 50 ambazo kila moja ilikuwa ikigharimu Sh50,000.

“Nilikuwa najua kabisa kuwa Dk kaachiwa ‘mzigo wa maana’ (kiasi kikubwa cha fedha) kwa ajili ya kukamilisha utafiti, lakini ikawa ni mbinde kila unapohitaji pesa kwa ajili ya utafiti. Majibu yake yalikuwa, we unasoma masters huna hela. Nenda katafute wafadhili,” anasema Yasin.

“Hata hivyo, nikapambana kufanya utafiti kwa sampuli angalau chache nipate cha kuandika. Lakini, tatizo likaja kila ninavyoandika anakosoa. Ukirekebisha anavyotaka anakosoa tena, mwishowe hujui uandike nini. Ilikuwa inafika wakati ukimfuata ofisini kwake unaomba Mungu usimkute maana ukimkuta hayo maringo na mpaka mkae mjadili ulichokiandika tena bila tija, basi sio leo. Ataingia huku atokee kule akutupie maneno haya, mara yale.

“Nakumbuka siku moja tukiwa ofisini alinichamba mbele za watu bila kujali heshima na utu wangu. Kwa kweli nilijisikia unyonge sana kama mwanamume mwenye familia, lakini nikawa sina namna. Kwa kweli nilijitahidi kuvumilia, lakini mwishowe nikamwambia Dk, naomba niruhusu nikafanye presentation na huko nitajitetea.

“…alichonijibu ni kwamba yeye hawezi kuwa mpumbavu akaruhusu upuuzi ule wangu ukasikilizwe na kujadiliwa mbele ya jopo. Basi mwishowe nikaona hii inakuwa ngumu. Huku kuna familia inahitaji kuhudumiwa, mwenyewe nahitaji pesa, kazi sina muda unazidi kwenda, basi nikaona ngoja nirudi zangu mtaani kuhangaika maisha yaendelee. Nikarudi darasani kufundisha na kwa kweli sikuwa na hamu tena ya kurudi huko.’’

Huyu ni mwathirika mmoja, lakini kisa chake kinasadifu masaibu na kadhia wanazopitia baadhi ya wanafunzi kutoka kwa wasimamizi wao.

Kibaya zaidi haya yanafanyika huku vyuo vingi nchini vikilia uhaba wa wahadhiri. Watu ambao kama wangehitimu pengine wangeweza kuziba pengo hilo, leo wanakoseshwa fursa sio tu ya kujiendeleza kitaaluma, lakini kulikosesha Taifa wataalamu bobezi katika fani mbalimbali.

Mkazi wa Dar es Salaam, Dk Diwani Msemo anashangazwa na namna mtoto wake anavyosotea kusoma shahada ya uzamili katika fani ya sayansi ya siasa na uongozi kwa miaka mitano sasa katika chuo kikuu kimoja kilichopo jijini humo.

Anasema mtoto wake na wanafunzi wenzake 10 walianza masomo tangu mwaka 2017.

Pamoja na kumaliza ‘course work’ ndani ya mwaka mmoja, hadi sasa hakuna kinachoendelea, akitaja sababu ni wasimamizi wa wanafunzi hao kuwa na mambo mengi.

“Wanajifanya wana vitu vingi. Mambo mengi ni pamoja na kusimamia kazi za wanafunzi. Kumweka mtu asome miaka minne, sio ndio kufanya shule ionekane kuwa ngumu,” anasema Dk Msemo.

“Research proposal (pendekezo la utafiti) eti ndio imepitishwa Julai. Kila siku supervisor (msimamizi) hana muda miaka imepita. Kweli ndio kuboresha elimu huko?’’


Wadau wafunguka sababu

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutoandikwa anasema, ni kweli tabia ya kufelisha au kuchelewesha wanafunzi ipo, lakini anawatupia lawama wanafunzi kuwa na uwezo mdogo, hivyo kushindwa kuhimili mikikimikiki ya usomaji wa shahada hizo.

“Siku hizi watu wengi wanachukulia masomo ya uzamili kama mtindo fulani wa maisha. Baadhi wanaamua kusoma bila kuwa na uwezo stahiki wa kumudu masomo hayo. Hali hii husababisha wao wenyewe kutokuwa na msukumo wa masomo na kuandika vitu visivyoeleweka na kuwafanya wasimamizi kukosa hamasa ya kusoma,’’ anafafanua.

Kuhusu udhaifu kutoka kwa wasimamizi, anasema wengi hawana motisha ya kuwasimamia wanafunzi, kwa sababu wanaona menejimenti za chuo hazithamini mchango wao.

“Msimamizi analipwa posho kidogo sana kwa mwaka mzima wa kumsimamia mwanafunzi, matokeo yake haweki kipaumbele katika usimamizi. Anatumia muda mwingi kufanya mambo yake binafsi, badala ya kusimamia kazi za wanafunzi,’’ anasema.

Pia, anasema wahadhiri wanafanya kazi katika mazingira magumu yasiyowapa ari kazini.

Sababu nyingine ya wanafunzi kuchukua muda mrefu masomoni anasema ni uhaba wa wahadhiri, huku waliopo wakilipwa masilahi madogo.

“Unakuta vyuo vinadahili wanafunzi wengi, lakini wahadhiri hawatoshi kusimamia kazi za wanafunzi hao. Mhadhiri mmoja anasimamia wanafunzi hadi 10 kwa mwaka katika hatua ya utafiti. Kwa hali hiyo hawezi kumudu kumaliza wote kwa wakati.’’