Mnyika ataka ‘amsha amsha’ Dar ianze kabla ya 2025

Katibu Mkuu wa Chadema,John Mnyika akizungmza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika maeneo ya Manzese jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amewataka wanachama wa chama hicho kutosubiri hadi mwaka 2025, badala yake; viongozi wawaongoze wananchi kudai utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ofisi zinazohusika.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amewataka wanachama wa chama hicho kutosubiri hadi mwaka 2025, badala yake; viongozi wawaongoze wananchi kudai utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ofisi zinazohusika.
Mnyika ameeleza hayo leo Jumamosi Agosti 26, 2023 wakati akihutubia wananchi wa kata ya Kibamba jimbo la Ubungo kwenye mkutano wa hadhara.
Amesema ni lazima kujiandaa kwa uchaguzi, kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kujenga mifumo wa Chadema Digitali, wagombea kujitokeza kufanya mafunzo na viongozi na kujipanga mapema kukiondo Chama cha Mapindiuzi (CCM) madarakani.
“Ni lazima kwa kuwa wametuchelewesha kwa miaka miwili, wakati tukisubiri kuwaondoa mwaka 2025 lazima Chadema kuanzia uongozi wa Mkoa, Kanda na Jimbo muwe sauti ya wananchi kwa sababu sauti ya watu ni sauti ya Mungu,” alisema Mnyika.
Mnyika ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Ubungo na Kibamba, alisema ili chama hicho kiweze kushika dola ni lazima kufanyike mabadiliko ya kisheria, kwani yapo mazungumzo yamefanyika yakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.
“Tunachokiona zimebaki siku chache kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, hakuna dhamira ya kupata katiba mpya wala kubadilisha sheria ya uchaguzi, tatizo tunaloliona liko kwenye Katiba,”
“Huwezi kutunga sheria ya mabadiliko ya vifungu bila kuigusa Katiba, sisi tunataka mambo mawili kwenye bunge lijalo, upelekwe mswada wa marekebisho ya sheria ili tuanze mchakato wa kupata katiba mpya. Lakini pia marekiebisho ya sheria ya Katiba ya sasa kwenye maeneo yote yanayohusu sheria za uchaguzi,” amesema.
Aidha Mnyika amesema uchaguzi wa Serikali za mitaa ni uchaguzi wa ‘hovyo’ kutokana na kanuni zake kutungwa na Waziri mwenye dhamana, hivyo kupelekea hata maeneo machache waliyowahi kushinda, kutumia nguvu kubwa.
Mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba Chadema, Earnest Mgawe, amesema, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, ubovu wa barabara na shida ya maji.
Amesema licha ya wananchi wa jimbo hilo kuvunjiwa nyumba zao kupisha mradi wa barabara ya njia nane kuanzi Kimara hadi Kibaha, hakuna aliyewahi kufidiwa.
“Chakushangaza baada ya Serikali kuwavunjia wananchi bila kuwalipa fidia, wameanza kuingia ubia kwa kuwapa maeneo ya wazi ambapo kumejengwa vituo vya mafuta,” alisema Mgawe.
Kwa upande wake aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Ubongo, Boniface Jacob, amesema mwaka 2015 ilipoanzishwa Halmashauri hiyo, iliongozwa na Chadema, ambapo majimbo yote mawili Ubungo na Kibamba walitekeleza miradi mbalimbali.
Alisema kwa kipindi kifupi walifanikiwa kujenga baadhi ya barabara, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu ambayo hawapo madarakani, bado barabara hasa za jimbo la kibamba zimekuwa ni mbovu.