VIDEO: Bosi wa Nida anavyopita katika tanuru la moto

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiwa kwenye foleni katika ofisi za Nida zilizopo Kawe jijini hapa jana, kwa ajili ya kujisajili ili wapate vitambulisho vya Taifa. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani Novemba 5, 2015 alifanya mabadiliko Nida kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa mkurugenzi mkuu, Dickson Maimu na watumishi wengine wanne wa mamlaka hiyo ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha kiasi cha Sh179.6 bilioni zilizotumika katika mradi wa Vitambulisho vya Taifa.Baada ya kuondolewa kwa Maimu, Rais Magufuli alimteua Dk Modestus Kipilimba ambaye alikaimu nafasi hiyo kwa miezi minane kabla ya kuteuliwa kuwa Mku-rugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).Baada ya Dk Kipilimba kuondoka Nida, nafasi yake ilikaimiwa na Andrew Mas-sawe aliyekaa kwa kipindi cha miaka

Moshi. Nani wa kulaumiwa kati ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) au watumiaji wa simu? Ni swali linalogonga vichwa vya wengi sasa zikiwa zimebaki siku nane tu simu zisizosajiliwa kwa alama za vidole kuzimwa nchini.

Kwa haraka, tatizo linaonekana liko kwa Nida katika ucheleweshaji wa kutoa namba za vitambulisho vya taifa au vitambulisho vyenyewe ili wananchi waweze kuzitumia kusajili laini zao kabla ya Januari 20.\

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitoa hadi Desemba 31 mwaka jana wamiliki wa laini za simu wawe wamezisajili kwa kutumia alama za vidole, lakini Rais John Magufuli akaongeza muda kwa siku 20 zaidi hadi Januari 20.

Wakati hayo yote yakiendelea hakuna ambaye hajainyooshea kidole Nida jambo linalomuweka bosi wa mamlaka hiyo katika kipindi kigumu.

Nida imenyooshewa kidole na viongozi mbalimbali wa juu wa Serikali, kuanzia Rais Magufuli, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, naibu wake Hamad Yusuf Masauni na viongozi wengine wa Serikali.

Katika ofisi za Nida sehemu mbalimbali nchini, kumeshuhudiwa foleni ndefu huku wananchi wakilalamikia usumbufu wanaoupata na kwamba hutumia siku nzima bila kufanikiwa kujisajili.

Kiini cha foleni ni wingi wa watu wanaohitaji namba za vitambulisho vya taifa kulinganisha na idadi ya wafanyakazi na vitendea kazi na wakati mwingine kompyuta zao kukosa mawasiliano.

Ni kutokana mkanganyiko wa kufungiwa simu zao, baadhi ya wadau wanaiona Nida kama imeshindwa kuwajibika na kuona kama mkurugenzi mkuu, Dk Kihaule aliyeteuliwa Oktoba 3 mwaka juzi na Rais Magufuli amekalia kuti kavu au yuko katika kipindi kigumu.

Mara kadhaa, Dk Kihaule amejikuta akipewa maagizo mbalimbali ya ghafla na viongozi wa juu serikalini jambo linaloashiria kuwa mambo si shwari katika mamlaka hiyo.

Maagizo ya Rais Magufuli

Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli alimtaka Dk Kihaule kufuatilia shughuli za utolewaji wa vitambulisho vya uraia nchi nzima.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo akiwa mkoani Morogoro baada ya wananchi wa Msamvu kumueleza adha wanazokumbana nazo wakati wa kujiandikisha kupata vitambulisho hivyo.

Rais Magufuli mbali na kumuagiza Dk Kihaule kwenda Morogoro kutatua changamoto hiyo, alisema tatizo linalowakabili wakazi hao huenda likawa linawakumba wananchi wengine maeneo mbalimbali nchini.

Baada ya wananchi kumueleza changamoto wanazokumbana nazo, Rais Magufuli alimpigia simu Dk Kihaule. “Nipo Morogoro hapa nimeelezwa tatizo la Nida, mna ofisi moja tu Mkoa wa Morogoro kwa nini? Mbona watu wa Kilosa wanakuja hapa wanapata shida.

“Sasa nisikilize mkurugenzi uko wapi uko Dar? Ondoka sasa hivi uje hapa Morogoro ushughulikie hili tatizo la Nida na ninataka watu walioko wilayani wasije hadi mkoani uje kutatua hili tatizo la Nida.

“Leo (Novemba 20 mwaka jana) uje hapa Morogoro ukae na mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ujipange ofisi yako izunguke wilaya zote ili wananchi wapate vitambulisho haraka,” alisema Rais siku hiyo.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alisema huenda tatizo linalowakabili wakazi wa Morogoro lipo maeneo mengine na akamtaka mkurugenzi huyo kuzunguka wilaya zote nchini.

Aprili 26, 2019, Rais Magufuli alitaka usajili wa laini za simu kwa alama za vidole uende sambamba na kazi ya utoaji wa vitambulisho na kuwataka TCRA na Wizara ya Mawasiliano kujipanga kwa hilo.

Desemba 27, 2019 wakati Rais akisajili simu yake alisema anaongeza siku 20 ili walioshindwa kusajili laini zao kwa sababu mbalimbali wafanye hivyo na muda huo hautaongezwa tena.

Pamoja na maagizo hayo ya Rais, tatizo linaonekana lipo pia kwa Nida, kwani kuna watu wengine wanalalamika kuwa inachukua hadi miezi mitatu mwananchi kupata namba tu ya kitambulisho cha Nida.

Januari 10, akiwa Songea mkoani Ruvuma, Waziri Lugola aliwatengua maofisa wa Nida wa mkoa huo kwa kukaa na vitambulisho 14,000 bila kuwajulisha wananchi. “Siwezi kukubali upuuzi huu ni lazima watu tukipeana kazi tuzitekeleze kwa manufaa ya wananchi na taifa hivyo hao maofisa vyeo vyao nimevitengua,” alisema. Lugola hakuishia hapo, akiwa mkoani Mtwara juzi, alikumbana na malalamiko ya wananchi dhidi ya Nida na kulazimika kumwagiza Dk Kihaule awe amefika Mtwara jana saa 2 asubuhi kutoa maelezo. Bosi huyo wa Nida aliitikia wito huo.

“Haiwezekani vitambulisho vya Nida ambavyo vinazalisha namba za utambulisho halafu Nida wanafanya mzaha na wanazembea,” alisema na kuwaonya watumishi wa Nida kujisahihisha.

Waziri Lugola aliyasema hayo baada ya kukuta ofisa mmoja wa Nida akiwa na vitambulisho 2,954 tangu Desemba mwaka jana, akiwa hajatoa taarifa kwa wamiliki wa vitambulisho hivyo ili wavichukue.

Januari 2, Naibu Waziri Masauni alitembelea kituo cha kuchakata taarifa za waombaji nchi nzima kilichopo Kibaha mkoani Pwani na kutoa maagizo kwa Dk Kihaule kuhakikisha anaongeza watumishi ili kwenda sambamba na siku 20 za nyongeza alizotoa Rais Magufuli.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata namba na vitambulisho vyao ndani ya siku 20. “Nimetembea vituo mbalimbali vya Nida nchi nzima, changamoto kubwa wanayotoa wananchi ni kwenda kila siku kufuatilia kitambulisho au namba katika kituo husika. Lakini wamekuwa wakipata majibu kwamba bado kipo kwenye mchakato, wakati mwingine ameomba miaka mitatu iliyopita sasa anapoteza muda na gharama kufuatilia.”

“Nimekuja hapa leo (Januari 2) nimegundua uchache wa watumishi, mkurugenzi ongeza watumishi. Ongezeni muda, wananchi wanafurika na kupata taabu, sisi ndiyo wawakilishi wao lazima tuwasemee na Rais ameshatoa maelekezo sasa ni utekelezaji tu,” aliagiza Masauni huku Dk Kihaule akisema watazingatia.

Wadau waitetea Nida

Pamoja na watu wengi kuinyooshea vidole Nida kwa sintofahamu ya utoaji vitambulisho, baadhi ya wadau wameitetea wakisema wa kulaumiwa ni wamiliki wenyewe wa laini za simu.

Ansi Mmasi wa Dar es Salaam aliyewahi kuwa meneja wa Vodacom alisema muda uliotolewa na TCRA ulikuwa mrefu wa kutosha, tatizo wananchi hawakuutumia vizuri muda huo. “Ilivyo kawaida wanatumia muda wa mwisho mwisho. Ushauri wangu mimi laini zizimwe hiyo tarehe 20 ila zisifutwe kwenye mfumo kwa miezi 12 na baada ya hapo ndio zifutwe,” alisema.

“Hiyo ndio namna nzuri ya kuwasukuma si tu wenye laini, pia Nida. Shinikizo la umma lina ufanisi zaidi kuliko viongozi. Inawezekana Nida wanakwazwa na viongozi hao hao,” alisisitiza.

Mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Mwanza na Moshi, Chriss Martin alisema anavyoona Nida wanafanya kazi nzuri ila wameelemewa kutokana na uchache wa vifaa. “Kwa mfano kuna wakati waliishiwa kadi. Maana yake ni nini, ni kwamba wanatakiwa wapewe fungu waagize. Wananchi waelezwe kuwa Nida ina upungufu wa vifaa na rasilimali watu,” alisema.

Mtaalamu mshauri wa masuala ya biashara, Conrad Kabewa alisema Nida hawana makosa ila wanahitaji taratibu madhubuti za kuwaongoza.

“Inachukuliwa kwamba Nida ni watoa vitambulisho jambo ambalo si sawa. Nida ni chombo cha kuwatambua raia Watanzania, ni kuwatambua kwa kukusanya taarifa zao zote muhimu.”

“Kuwashinikiza watoe vitambulisho bila kupata taarifa za watu ni kuruhusu watu wasio raia wa Tanzania wapewe vitambulisho vya uraia. Suala la usajili wa raia haliwezi kuwekewa ukomo.”

Kabewa alishauri kuwa kila anayefikisha miaka 18 asajiliwe na kazi hiyo isiwe na ukomo na kutaka usajili wa laini za simu usitolewe muda mfupi wakati utambuzi wa raia unachukua muda.