Kesi kupinga tozo miamala ya simu yaunguruma

Saturday August 07 2021
tozopic
By Ephrahim Bahemu

Dar es Salaam. Wakati umma ukisubiri kwa hamu kusikia hatma ya tozo ya miamala ya simu kutoka serikalini, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetoa mwenendo wa kesi yake kikisema itasikilizwa kwa mara nyingine Agosti 16 mwaka huu.

Agosti Mosi, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na mwenzake wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Faustine Ndugulile waliwasilisha taarifa ya timu ya mapendekezo ya namna bora ya utozaji wa tozo za miamala ya simu kwa Waziri Mkuu kama ilivyoelekezwa na Rais samia Suluhu Hassan, lakini hadi sasa inasubiriwa taarifa au hatua juu ya hatua inayofuata.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba, timu hiyo inajumuisha wataalamu kutoka Benki Kuu, pia watakuwapo wa kutoka Mamlaka ya Mwasiliano Tanzania (TCRA), Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Wakati kinachofuata kikisubiriwa, taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga ilisema kesi hiyo kwa mara ya kwanza ilisikilizwa Agosti 5, 2021 mbele ya Jaji John Mgeta.

“Siku ya tarehe 27/07/2021 LHRC kilifungua shauri namba 11 la mwaka 2021 kuomba mapitio ya mahakama kuu kuhusu sheria ya mfumo wa taifa wa malipo pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu,” ameeleza katika taarifa hiyo.

Henga alisema kesi hiyo ilifunguliwa kufuatia kupitishwa kwa mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 na sheria ya fedha iliyosababisha kuweka tozo ambayo anaitaja kuwa mzigo kwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara ndogondogo.

Advertisement

Soma zaidi: Mwigulu atoa ufafanuzi tozo za simu, majengo

Katika bajeti kuu iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni mwaka huu, na kuanza kutumika Julai mosi Serikali ilianzisha tozo ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kutuma na kutoa pesa jambo ambalo liliibua kilio kwa wananchi huku watoa huduma za simu wakisema biashara ya huduma hiyo itazorota.

Julai 27, 2021 Rais Samia Suluhu akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tozo hizo alisema suala la tozo za miamala ya simu lipo palepale lakini Serikali inakwenda kuangalia njia ya kulitekeleza na kesho itapokea maoni ya kamati iliyoundwa kutathimini suala la tozo mpya za miamala ya simu.

Alisema baada ya kuanza kwa tozo kelele zilikuwa nyingi na kwakuwa Serikali ni sikivu ikapokea maoni kisha akawataka mawaziri wa mawasiliano na fedha kukutana.

Soma zaidi: Maumivu ya tozo miamala ya simu

“Makato haya tuliyaweka kwa nia njema tu, nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa lakini wakivuna wanashindwa kutoa mazao yaliko kuleta kwenye maeneo ya masoko, tatizo ni njia za vijijini hakuna, kwa hiyo sehemu kubwa ya fedha hizo inakwenda kujenga njia za vijijini,” alisema Rais Samia.

Soma zaidi: Kiini tozo za simu zilizozua mjadala

Alisema njia hizo zitawasaidia wakulika kufikisha mazao sokoni na kufaidi jasho lao na bidhaa zisiharibike kabla ya kufika sokoni. Vilevile alisema maeneo mengi yana changamoto ya maji kwakuwa asilimia 26 bado haijafikiwa, fedha hizo pia zinakusudiwa kupelekwa kwenye miradi ya maji.

“Niwaambie Watanzania tumesikia vilio, tunakwenda kuangalia njia nzuri ya kwenda na hili lakini hizi tozo nataka niseme zipo, ila tutaangalia njia nzuri ambayo haitaumiza watu, serikali ipate na maendeleo yaendelee,” alisema.

Julai 26, 2021 Mwenyekiti wa chama cha waendesha huduma ya simu za mkononi Tanzania, Hisham Hendi alisema wateja zaidi ya milioni moja walisitisha kutumia huduma za miamala ya simu.Advertisement