Kifo cha Magufuli kilivyotoa funzo usiri, mifumo

Muktasari:

  • Aprili 4, 1841, usiku, Marekani kwa mara ya kwanza walimpoteza Rais akiwa madarakani. Ni William Henry Harrison. Alikaa madarakani kwa siku 31 tu.


Dar es Salaam. Aprili 4, 1841, usiku, Marekani kwa mara ya kwanza walimpoteza Rais akiwa madarakani. Ni William Henry Harrison. Alikaa madarakani kwa siku 31 tu.

Harrison, aliapishwa kushika madaraka ya urais Machi 4, 1841, kisha Aprili 4, 1841, akaitikia wito wa Mungu, kwamba kila nafsi itaonja mauti.

Zingatia, Aprili 4, 1841, dunia ilikuwa ya kijima mno. Hata ugunduzi wa mawasiliano kwa njia ya waya (telegraph), ulikuwa bado. Barua ndio yalikuwa mawasiliano ya kisasa zaidi.

Magazeti ndiyo yalikuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano kwa umma. Kazi za ugunduzi wa simu zilizoanzishwa na Muitaliano Antonio Meucci, Mfaransa Charles Bourseul na Mskotishi, Alexander Bell, zilifuata baada ya kifo cha Harrison.

Meucci jaribio lake lilikuwa mwaka 1849, yaani miaka nane baada ya kifo cha Harrison. Bourseul ni mwaka 1854, wakati mafanikio ya Bell kuiunganisha dunia kwa waya, yalitokea mwaka 1876. Kisha simu ya kwanza ikaanza kazi mwaka 1877.

Sasa, Rais Harrison alifikwa na mauti akiwa Washington DC, wakati huo Makamu wa Rais, John Tyler, alikuwa Williamsburg, Virginia, kwa ziara ya kifamilia.

Asubuhi, Aprili 5, 1841, Tyler alipokea ujumbe wa maandishi kutoka White House, kumjulisha kuhusu kifo cha Harrison. Siku hiyohiyo (Aprili 5, 1841), taarifa ilitolewa. Aprili 6, 1841, magazeti yaliripoti kifo cha Harrison.

Hiyohiyo Aprili 6, 1841, Tyler akakutana na Baraza la Mawaziri. Akala kiapo cha urais mbele ya mawaziri wote. Akaanza kazi. Kipindi hicho hata Katiba ya Marekani haikuwa inampa Makamu wa Rais haki ya kurithi kiti baada ya Rais kufa, kujiuzulu, kupoteza uwezo wa kuongoza au kufukuzwa.

Kwa Marekani, walivuka salama changamoto ya kifo cha rais wa kwanza aliye madarakani kwa sababu ya mifumo imara. Walivuka mtego wa kikatiba kuhusu urithi wa rais kwa kuwa mifumo ilisimama imara kwenye kipindi kigumu.

Miaka 180 baadaye, Tanzania yenye umri wa miaka 59, inaondokewa na Rais aliye madarakani. Ni Dk John Magufuli. Unatokea utata mkubwa wa taarifa za hali ya afya ya Rais.

Kipindi ambacho dunia imekuwa sawa na kijiji kidogo, mawasiliano ni rahisi mno. Ukaibuka udhaifu mkubwa. Mpaka leo hayajatolewa majibu; kwa nini ilikuwa vile. Ilitokeaje? Ukweli ni upi?

Taarifa zikaanza kutolewa mitandaoni kuwa Rais Magufuli alikuwa na hali mbaya kiafya. Ikaelezwa alifikishwa mpaka Kenya. Wapo waliodai alipelekwa India.

Kipindi hicho taarifa zinavumishwa, taifa likageuka jukwaa la propaganda. Maudhui ni afya ya Rais Magufuli. Waliomnenea ugonjwa wakanena. Waliopaza sauti kwamba alikuwa na siha njema, walisema.

Kuna mtu anaitwa Evarist Chahali, yeye hujitambulisha kama mtumishi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa na alishapata kufanya kazi ya uchambuzi wa masuala ya siasa na jamii kwenye magazeti kadhaa nchini. Chahali ndiye alikuwa wa kwanza kusema Rais Magufuli alishafariki dunia.

Chahali akaeleza kuwa taarifa za Rais Magufuli kupelekwa India hazikuwa za kweli, bali alifia Hospitali ya Viongozi, Mzena, Kijitonyama, Kinondoni, Dar es Salaam.

Wakati mitandao ikipaza sauti kwa taarifa mbili, za kifo na kuugua, upande wa pili, kulikuwa na jitihada nyingi za kukanusha uvumi huo. Kuna wakati zikawa zinasambazwa picha mnato na video za Rais Magufuli, za zamani, ili kuonesha alikuwa vizuri akichapa kazi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Rais Magufuli alikuwa Ikulu akichapa kazi. Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, aliuambia umma kuwa yeye huzungumza mara kwa mara na Rais Magufuli, hivyo alikuwa mzima na salama.

Machi 14, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, wakati huo akiwa Makamu wa Rais, alifanya ziara Tanga na akiwa Pangani, alisema, kukaguliwa mafua na homa ni kitu cha kawaida.

Ni kusema, baada ya mengi, Samia kwa mbali alikiri Magufuli kuumwa. Hata hivyo, namna ilivyoelezwa ni taarifa kuwa hakuwa kwenye hali ya hatari.

Machi 17, mwaka huu, saa 5 usiku, Rais Samia alilihutubia taifa, kulitaarufu kifo cha Magufuli. Kwamba kilitokea siku hiyo, Hospitali ya Mzena, Kijitonyama.


Tujadili bila jazba

Baada ya Rais Samia kutangaza kifo cha Magufuli, kuna jambo moja tu huwezi kupinga; mitandao haikuwa ikisema uongo kwa asilimia 100.

Mitandao ilisema Magufuli alikuwa anaumwa. Pamoja na kukanusha, baadaye ikaelezwa kweli aliumwa. Mitandao ikasema Magufuli alifariki dunia. Na kweli, Mungu akamchukua.

Viongozi wa Serikali walikanusha kuwa Magufuli hakuwa akiumwa, baadaye ikabainika kweli alikuwa mgonjwa. Wakakemea taarifa za kifo, kisha ikatangazwa ameshafariki dunia.

Tuulizane kwa akili bila hisia; upande upi unaweza kuaminika mpaka hapo? Waliosema uongo ambao uligeuka ukweli? Au walioupinga uongo lakini wakaja kuthibitisha ule uongo umekuwa kweli?

Ndiyo, taarifa ya Serikali lazima itafsiriwe ndio ukweli wenyewe. Na chochote kinachotoka nje ya mfumo, kikipingwa na mfumo, kinakuwa uongo. Kwa maana hiyo, taarifa za ugonjwa na kifo cha Magufuli, zilizotoka mitandaoni ni uongo uliogeuka kweli.

Taarifa kutoka kwa viongozi wa serikali kuhusu afya ya Magufuli ni ukweli uliogeuka uongo. Na hapa ieleweke kuwa naamini kweli Majaliwa alikuwa mkweli aliposema Magufuli alikuwa Ikulu akichapa kazi. Hata Chalamila pia alipodai kwamba walikuwa wakipigiana simu na Magufuli.

Tukiwa wakweli, utaona kuwa watu wa mitandao ni rahisi kuaminika kwa sababu walichokisema ndicho baadaye kikawa kweli. Viongozi wa serikali hata kama walichokuwa wanakisema kilikuwa kweli kwa asilimia 100, ni vigumu kuaminika.

Katika somo la falasafa za tabia kimaadili na thiolojia (consequentialism), inafundishwa kuwa yale matokeo ya mwisho ndio huamua ukweli au uongo. Na kuna msemo unaoendana na falsafa ya consequentialism kuwa “end justifies the means” – “Tamati hudhihirisha mantiki”.

Je, mwisho kabisa, kifo cha Magufuli kilifanya upande gani uonekane ndio uliokuwa na mantiki? Waliozusha mitandaoni au waliokanusha na kunyoosha ukweli kwamba Magufuli alikuwa akichapa kazi Ikulu?

Somo la falsafa za tabia kimaadili na thiolojia (consequentialism). Inafundishwa kuwa yale matokeo ya mwisho ndiyo huamua ukweli au uongo. Na kuna msemo unaoendana na falsafa ya consequentialism kuwa “end justifies the means” – “Tamati hudhihirisha mantiki”.

Je, mwisho kabisa, kifo cha Magufuli kilifanya upande gani uonekane ndio uliokuwa na mantiki? Waliozusha mitandaoni au waliokanusha na kunyoosha ukweli kwamba Magufuli alikuwa akichapa kazi Ikulu?


Tatizo la mifumo

Kuna jambo halibishaniwi; ni Rais Magufuli kuumwa na kufa na kwamba mifumo haikutaka taifa lijue wakati mitandao ilipokuwa inapaza sauti. Hata hivyo, mwishoni ikadhihirika ni kweli.

Kwa kila kilichotokea na kwa kurejea falsafa ya consequentialism kwamba “end justifies the means” – “tamati hudhihirisha mantiki”, utakubali kuwa watu wa mitandao hawakuwa wakinena uzushi mtupu.

Kwa sehemu kubwa kama si asilimia 100, wao ndio walikuwa wakitoa taarifa zenye ukweli (hii ni kwa mujibu wa ukokotoaji wa consequentialism). Kama ndivyo, walikuwa wanatoa taarifa wapi ikiwa mifumo ilitaka hali ya Rais Magufuli iwe siri?

Ukifika hapo, hutapata shida kusadiki kwamba watu wa mitandao walikuwa na taarifa za ndani na wakawa wanazitoa kwa umma kinyume na matakwa ya mifumo. Je, iliwezekana vipi?

Jibu ni kwamba ndani ya mifumo hakuna uwezo wa kutunza siri. Taarifa ambayo mifumo haikutaka itoke nje, ikatoka na ikazagaa mitaani. Wananchi kwa wingi wao wakawa wanangoja tamko kama yasemwayo ni kweli au la!

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, alipokuwa akitoa hotuba yake ya tanzia ya kifo cha Magufuli, Chato, Geita, alisema alipoambiwa “Magufuli kafa”, aliuliza mara mbilimbili kama ni kweli imethibitishwa au ndio yaleyale maneno ya mitandao.

Kikwete alisema, alipojibiwa kwamba tangazo lilitolewa na Rais Samia, ndio akaamini. Utaona kuwa Kikwete mwenyewe alishaona kulikuwa kuna kuyumbisha taarifa kwa kiasi kikubwa.

Na kwa vile yaliyosemwa na mitandao ndio yalikuja kuthibitishwa ni kweli, maana yake kama mifumo ilikosa usiri, basi kulikuwa na mgawanyiko mkubwa. Sehemu ya mifumo ilitaka iwe siri upande mwingine waliamua kuvujisha mitandaoni. Ndivyo inaonekana.

Taifa lenye mifumo yenye mgawanyiko ya ndani kwa ndani hutambuliwa kwa fragile state (dola dhaifu). Uwezo wake wa kulinda raia huwa mdogo. Taifa imara ni lile ambalo kinazungumza lugha moja mbele ya uso wa jamii.

Ukiacha hayo maeneo ya umma kulikuwa na mgawanyiko wa mifumo au usaliti wa ndani kiasi cha kupindisha taarifa, kuna jambo la aibu; ni jinsi viongozi wa serikali walivyokuwa wanatoa taarifa ambazo kwa sehemu kubwa zimetafsiriwa kuwa hazikuwa kweli.

Je, mifumo iliwayumbisha mpaka viongozi wakawa hawaelewi ukweli ni upi na wakatoa taarifa ambazo baadaye zikaonekana zilikosa usahihi au walichokisema ni kweli ila muda ukageuza uongo kuwa ukweli.

Ndio, muda huweza kubadili kila kitu. Pengine waliokuwa wakisema Magufuli anaumwa au alikuwa ameshafikwa na mauti, walikuwa waongo na wakaamini uongo wao ndio ukweli kama ilivyo kanuni ya “illusory truth effect”, kwamba uongo ukirudiwa mara kwa mara huchukuliwa ndio ukweli.

Hata hivyo, baada ya mamlaka kutangaza kifo cha Maguful, Samia akaapishwa kuwa Rais, halafu Magufuli akazikwa, utakuwa na ubavu upi wa kusema yaliyosemwa mitandaoni ni illusory truth effect?

Kingine ni nafasi ya Rais. Hapa nchi ilikosewa sana. Rais ni mali ya umma. Wananchi ndio humwajiri Rais kupitia sanduku la kupigia kura. Na kwa kawaida, mwajiri huhitaji taarifa za mahali alipo mfanyakazi wake.

Kifo cha Maguful kilitengeneza tamthiliya ya ajabu kwa sababu mifumo haikutaka kuheshimu uwazi kati ya Rais na wananchi waliompa ajira. Afya ya rais lazima isemwe. Na matarajio yaelezwe.

Hivi karibuni, Rais wa Marekan, Joe Biden, aliandika barua kukabidhi mamlaka ya urais kwa Makamu wa Rais, Kamala Harris, ili aakashughulike na matibabu. Akaahidi kurejea ofisini baada ya hali yake kuwa imara. Umma wa Wamarekani ulielezwa hivyo.

Makosa yaliyofanyika kipindi cha kuugua na kifo cha Magufuli, hayapaswi kurejewa. Watanzania hawatakiwi kunyimwa taarifa za maradhi au kifo cha rais ili wajue kwa wakati rais anaugua au amekufa nchi inaongozwa na nani?

Kuweka yote kwenye kapu moja, bila shaka, mifumo ya nchi ilikosa weledi kwa kiasi kikubwa katika kushughulikia ugonjwa hadi kifo cha Magufuli.