Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polepole aibua tuhuma nzito, aitwa kujieleza

Balozi Humphrey Polepole anayeiwakilisha Tanzania nchini Cuba.

Muktasari:

Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole ameibua tuhuma nzito zinazoashiria mvutano ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huku leo akiitwa kuhojiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Dar es Salaam. Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole ameibua tuhuma nzito zinazoashiria mvutano ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huku leo akiitwa kuhojiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Polepole amekuwa akitumia kipindi chake cha “Shule ya Uongozi” kwenye chaneli yake ya YouTube, kueleza fikra zake na kupinga mambo kadhaa yanayoonekana kuwa kinyume cha msimamo wa CCM na Serikali.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, Polepole alisema kupitia kipindi hicho, amekuwa akipokea vitisho na kutakiwa kuachana na kipindi hicho huku wengine aliowaita “wazee” wakimsihi akae kimya.

Kada huyo wa CCM alisema ameitwa na CCM kuhojiwa kutokana na kile alichokiita tuhuma dhidi yake.

Alisema hayo yote yametokana na yeye kuamua kuzungumza na kutotii amri ambayo amekuwa akipewa ya kukaa kimya.

“Hii tabia ya watu wananiambia nikae kimya...nitaakaje kimya, nina uhuru wa kuzungumza. Nimehangaika na hii ‘kaa kimya’, niliitwa kwenye chama na yaliyozungumzwa huko ni siri na nilishasema sitayaeleza hadharani.

“Niseme tu niliitwa huko kwa kuwa nilikuwa na tuhuma, lakini nilizijibu zote, moja baada ya nyingine na kwa unyenyekevu mkubwa. Juzi nimesema naanza msimu wa pili wa Shule ya Uongozi, nimepokea mashtaka, yaani nimeshtakiwa na Jamhuri,” alisema Polepole.

Septemba 3, kamati ya maadili ya wabunge wa CCM ilimhoji Polepole kutokana na msimamo wake wa kupinga chanjo ya Uviko-19, huku msimamo wa Serikali na chama chake ukiwa ni kuhamasisha wananchi wapate chanjo hiyo.

Desemba 18, mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa utafanyika ukitanguliwa na kikao cha Kamati Kuu na huenda moja ya ajenda katika kikao hicho ikawa ni kupokea taarifa ya kamati ya maadili baada ya kumhoji mbunge huyo.


CCM yamvutia pumzi

Alipoulizwa kuhusu tuhuma za Polepole anayedai kusumbuliwa na wahuni ndani ya CCM, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, kanali mstaafu Ngemela Lubinga alisema chama ni taasisi na hakina shida na matatizo ya mtu mmoja mmoja.

“Yeye hayo ameyaeleza, ndiyo mtazamo wake lakini chama chenyewe kinaendelea na kuongeza wanachama…chama kinajua Polepole ni mwanaCCM, kama anataka kutoka, chama kinaendelea na shughuli zake,” alisema Lubinga.

Kuhusu chama kumchukulia Polepole hatua za kinidhamu, Lubinga alisema hayo mambo yanashughulikiwa na kamati ya maadili, hivyo kama wataona kuna haja ya kufanya hivyo, watachukua hatua.


Aitwa kuhojiwa TCRA

Katika mkutano wake wa jana, Polepole alisema amepokea barua kutoka TCRA inayoeleza kwamba yeye ni mshtakiwa wa kwanza mwaka huu, jambo alilosema limemshangaza kwa sababu alilipa fedha kupata leseni ya kurusha maudhui, hivyo hadhani kama anaweza kupangiwa cha kusema.

“Nimepokea wito. Jumatatu nitawasilisha utetezi wangu kwa TCRA, nitakwenda kuyafafanua kwa kina.”

Polepole alisema kumekuwa na sintofahamu kuhusu kauli zake huku wengine wakimweleza kuwa aache kuongelea Shule ya Uongozi, jambo alilosema hawezi kuacha.


TCRA wamsubiri

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkurugezi Mkuu wa TCRA, Jabir Bakari alikiri kumuandikia barua ya wito Polepole na atakwenda kuhojiwa na Kamati ya Maudhui ya TCRA.

Hata hivyo Bakari hakutaka kueleza kwa kina tuhuma zinazomkabili mbunge huyo, akisema mwenyewe ndiye yuko kwenye nafasi ya kueleza.

Bakari alisema TCRA inashughulika na watu waliopewa leseni ili kutoa huduma na leseni hiyo inaambatana na masharti ambayo mhusika anatakiwa kuyafuata.

“Sisi tuna-deal na licensees (tunashughulika na wenye leseni)…leseni ina masharti, kwa hiyo hatu-deal na individual, tuna-deal na licensee na hatushughuliki naye kutokea hewani, tunashughulika naye kulingana na kitu anachotakiwa kufanya kwenye leseni,” alisema.


Vitisho anavyovipata

Polepole, ambaye kwa miaka mingi alikuwa mwanaharakati, alisema amekuwa akipokea vitisho na kauli za kumvunja moyo kutoka kwa baadhi ya wazee na kusema kwamba hatawajibu kwa kuwa wanatumia uhuru wao.

“Nimetishwa kwamba nitanyang’anywa ubunge nisipoacha Shule ya Uongozi. Ubunge nimeupata mwaka jana, hapa Dar nimekuja kitambo na niliingia CCM tangu mwaka 2020.

“Ijapokuwa kumekuwa na migogoro ya hapa na pale sijali na licha ya kwamba wameuchukua uenyekiti wangu katika Kamati za Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai sina matatizo naye,” alisema.

Aliweka wazi kuwa ijapokuwa kumekuwa na kelele nyingi kuhusu yeye hana mpango wa kuondoka CCM na hatarajii hilo.

“Niliingia CCM mwaka 2000, nikapiga kura kwa mara ya kwanza kwa kutaka mwenyewe, sitatoka. Kama ninatoka kuna mapambano yametokea labda wanibebe mpera mpera...Ukiona nimetoka watu wenye nguvu walinitolea dirishani.

“Mie sijali. Sijavunja sheria na katiba ya nchi, siwazi, sina fikra, hata kama nitagharamika kwangu ni ushindi, mimi Mkristo tena mlokole sidhani nitagharamika kwa kuusema ukweli. Niliingia CCM kwa hiari na nitatoka kwa hiari,” alisema Polepole.

Kutokana na kauli zake amekuwa akijitofautisha na wengi. Polepole alipoulizwa iwapo CCM kuna makundi alisema makundi ni sehemu ya uhuni na chama hicho kinatakiwa kuwa wamoja.

“Mhuni ni mhuni tu hawabadiliki, nitoe rai kwa viongozi wawe macho na wahuni, awamu ya jana alitukana Serikali leo anakaa upande wa Serikali.

“Na hili la wahuni nililizungumza sana, ni wale wanaokwepa kodi utawapata ukienda TRA, wabadhirifu wa mali za umma wapo, kazi yetu kama viongozi wa taifa ni kuwathibiti.

“Sasa naongea mtu mwingine anaibuka. Hivi mimi niite wahuni halafu mtu na akili zake timamu anasimama na kujijumuisha au kufurahia? Niseme wazi watu wakizingua mahala natoka tena nazungumza. Nitatumia kila fursa kuhakikisha na mimi natumia nafasi yangu kushughulika na wahuni,” alisema Polepole.

Polepole alisema anashangazwa na baadhi ya watu waliokuwa wakiipinga Serikali ya CCM hivi sasa wanaishangilia na kumsifu Rais Samia Suluhu Hassan kana kwamba hakuwepo wakati wa utawala wa Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu alisema