Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali, Mtikila walivyotoana jasho katika kesi ya mgombea binafsi-2

Serikali, Mtikila walivyotoana jasho katika kesi ya mgombea binafsi-2

Muktasari:

  • Katika toleo la jana la mapitio ya kesi za kutaka wagombea binafsi waruhusiwe kwenye urais, ubunge na nafasi nyingine tuliona jinsi mwanasiasa machachari, Christopher Mtikila alivyoanza safari ya kutetea alichokiamini kuwa ni haki ya kikatiba kwa kuiomba mahakama iruhusu wagombea binafsi.
  • Tuliona Mtikila alivyoshinda kesi hiyo ya kwanza 1994 baada ya kufunguliwa mwaka 1993 ushindi uliodumu kwa muda mfupi kisha Serikali kupeleka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yaliyozuia tena wagombea binafsi.
  • Hata hivyo, Mtikila hakukata tamaa. Alirudi tena Mahakama Kuu kuiomba itamke kuwa mabadiliko hayo ya sheria yalikiuka vifungu vya Katiba na ni kinyume na matamko na makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za msingi za binadamu ambayo Tanzania imeyaridhia. Endelea…

Kutokana na Mtikila kupinga mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1994 yaliyozuia wagombea binafsi nchini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) aliyapinga maombi hayo.

AG alisema kupitishwa kwa Sheria namba 34 ya mwaka 1992 pamoja na mabadiliko ya katiba yalikuwa halali, sahihi kisheria kwa manufaa ya umma na hayakukiuka haki za msingi za binadamu kama alivyosema Mtikila.

Mbali na hilo, AG alieleza mabadiliko hayo ya Katiba hayakuwa ya kibaguzi kwa kuwa sheria zinafanya kazi sawa kwa watu wote wakiwamo wagombea wa kisiasa.

Kwa kifupi, msingi wa mvutano kati ya wadaiwa katika maombi hayo ulikuwa ni kama mabadiliko ya Katiba yaliyoletwa na Sheria namba 34 ya 1994 yalikuwa kinyume na Katiba.

Majaji watatu walisikiliza maombi hayo ambao ni Amir Manento (wakati huo Jaji Kiongozi), Salum Massati na Thomas Mihayo walijielekeza kuamua mambo matatu.

Kwanza, kama Ibara ya 39 (1) (c) na 39 (2) na Ibara ya 67 (b) na 67 (2) (e) zilikuwa kinyume cha Katiba. Pili, walilenga kuamua endapo vifungu hivyo vilikidhi kipimo cha uhalali, na mwisho, kama mabadiliko hayo yalikiuka makubaliano na mikataba ya kimataifa yaliyoridhiwa na kusainiwa na Serikali ya Tanzania.

Mapambano wa hoja

Katika hatua za awali za usikilizaji wa shauri hilo, pande zote ziliamriwa kuwasilisha hoja zao kwa maandishi halafu mawakili walipewa fursa ya kufafanua zaidi hoja zao za maandishi kwa mdomo.

Mtikila aliwakilishwa na Richard Rweyongeza na Mpale Mpoki huku Serikali ikitetewa na Wakili wa Serikali Mkuu, Matthew Mwaimu na Ndunguru.

Mawakili wa Mtikila waliieleza mahakama kuwa mabadiliko ya Ibara ya 39 na 67 yaliyozuia haki ya raia kugombea urais na ubunge yalikiuka haki za msingi zilizoainishwa katika Ibara ya 21 (1) ya Katiba zinazowapa haki ya kufanya umoja na ilikiuka Ibara ya 20 (4) ya Katiba inayozuia kupitishwa kwa sheria inayolazimisha watu kujiunga na jamii au jumuiya yeyote.

Rweyongeza na Mpoki walisema vifungu vya sheria wanavyovipinga vimeweka ukomo kwa raia wanaotaka kugombea nafasi za kisiasa kufanya hivyo.

Walisea sheria hizo zinawabagua raia ambao ni wanachana wa vyama vya siasa dhidi ya wale ambao si wanachama wa vyama vya siasa linapokuja suala la kugombea katika uchaguzi.

Mawakili wa Mtikila waliendelea kueleza kuwa kwa kuwa tayari Jaji Kahwa Lugakingira alizitambua haki za msingi (fundamental rights) katika Katiba, mabadiliko yaliyoletwa na Sheria namba 34 ya 1992 hayakuwa tena na nguvu kisheria.

Wakifafanua endapo kutungwa kwa sheria inayoweka ukomo wa kufurahia haki zinazolindwa na Katiba kunahalalishika au la, Rweyongeza na Mpoki walisema ni wajibu maombi kuthibitisha kuwa sheria hiyo inayopingwa inakidhi kipimo cha kuhalalishika.

Mwisho, Rweyongeza na Mpoki walidai Sheria namba 34 ya 1992 ilikiuka Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu. Walisema matamko hayo lazima yazingatiwe katika kutafsiri haki na wajibu muhimu.

Katika kuipambania Serikali, Maimu na Ndunguru walisema mabadiliko ya Katiba yanayopingwa yalifanywa ndani ya uwezo wa kisheria wa Bunge na hayakukiuka kifungu chochote cha Katiba.

Kwa sababu hiyo, waliegemea katika Ibara ya 98 (1) na (2) ya katiba inayosema Bunge linaweza kutunga sheria ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba ikiwamo kurekebisha au kusahihisha au kufuta mashari hayo na kuweka mengine au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.

Wakijibu endapo mabadiliko ya sheria yanayopingwa na Mtikila yalikiuka Ibara ya 21 (1) ya Katiba, mawakili hao wa Serikali walieleza kuwa yalifanyika kwa nia njema.

“Zuio la wagombea binafsi katika uchaguzi mkuu na wa Serikali za Mitaa ni njia ya kufikia demokrasia ya uwakilishi (representative democracy). Kimsingi, Katiba inalenga kuanzisha na kulinda demokrasia ya uwakilishi ambayo ni sera inayofuatwa na nchi yetu kwa lengo la kulinda amani, utulivu, usalama na maelewano,” walieleza mawakili hao. “Kanuni inayomtaka mtu anayetaka kugombea nafasi ya uongozi kufanya hivyo kupitia chama cha siasa inalenga kuhakikisha yeyote anayeteuliwa kuwa mgombea anajulikana vizuri kwa watu anaotaka kuwaongoza,” walisisitiza.

Wakijibu hoja kuwa mabadiliko ya sheria yanayobishaniwa yalikuwa ya kibaguzi, mawakili hao walisema yaliwalenga wanaotaka kuwania nafasi za uongozi kwa kuwa kanuni ya usawa hailazimishi kila mtu atendewe sawa na mwingine lakini watu walio katika nafasi sawa ndio watendewe sawa.

Wakanukuu kesi ya Afrika Kusini kati ya Jamhuri ya Afrika Kusini dhidi ya Hugo (1997) wakisema wakati mwingine inawezekana kuhalalisha ubaguzi kama jambo la kipekee kama nia ni kukamilisha nia njema wakiiita kanuni ya ubaguzi unaokubalika (principal of fair discrimination).

Mwaimu na mwenzake pia walieleza kuwa Ibara ya 21 (1), 39 (1) (2), 67 (1) (b) na Ibara ya 20 (4) kama zikisomwa pamoja, itaonekana wazi kuwa Ibara ya 21 (1) haitengenezi utaratibu wowote unaohusiana na haki ya mtu kupiga au kupigiwa kura.

Walidai utaratibu wa mtu kupiga au kupigiwa kura upo katika Sheria ya Uchaguzi na Kanuni zake.

Walisema kuna wasiwasi kuwa vifungu hivyo vya sheria vinaweza kutumiwa vibaya na kuifunga haki ya kuongoza kwa watu wachache na kuifanya ndoto ya kujenga jamii ya kidemokrasia isiwe ya uhakika.

Mwisho, mawakili hao walidai ingawa hawipingwi kuwa Tanzania imetia saini na kuridhia Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu, matamko ya makubaliano hayo yana kikomo.

Walitolea mfano wa Ibara ya 29 (2) ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu ambalo limeweka wazi kuwa utekelezaji wa haki zilizoainishwa katika tamko hilo utafuata ukomo uliowekwa na sheria kwa nia ya kulinda na kutambua haki na uhuru wa wengine.

Usikose toleo la kesho kuona jinsi majaji walivyochambua hoja za pande zote mbili na kutoa majibu.