Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vidonge vya P2: Matumizi holela na hatima usalama wa wazazi wa kesho

Vidonge vya P2: Matumizi holela na hatima usalama wa wazazi wa kesho

Muktasari:

  • Wakati vijana wakifanya ngono zembe wakiamini dawa za dharura za kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu P2 ndiyo mkombozi wao, imebainika zikiendelea kutumika kiholela zitasababisha madhara kwao na hasara kwa Taifa miaka ijayo.

Wakati vijana wakifanya ngono zembe wakiamini dawa za dharura za kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu P2 ndiyo mkombozi wao, imebainika zikiendelea kutumika kiholela zitasababisha madhara kwao na hasara kwa Taifa miaka ijayo.

Matumizi ya vidonge hivyo (Postinor-2) yamesababisha kutozingatiwa kwa matumizi ya kondomu, hali inayowaweka vijana katika hatari ya kupata Virusi vya Ukimwi (VVU), homa ya ini, magonjwa ya zinaa, saratani na ugumba.

Kujikinga na mimba kwa kumeza P2 kumetajwa huenda kutaongeza idadi ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wenye VVU, hali itakayoilazimu Serikali kuongeza afua za kupambana na maambukizi hayo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto miaka michache ijayo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wasichana wawili mpaka watatu wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24 huambukizwa VVU kila baada ya saa moja nchini.

Maambukizi ya VVU yanaenea kwa kasi zaidi kwa kundi la wasichana balehe wenye umri huo kwa asilimia 2.1 ikiwa ni mara tatu zaidi ya vijana wa kiume kwa asilimia 0.6.

Hayo yameelezwa na wataalamu wa masuala ya afya ya uzazi kwa vijana, walipozungumza na Mwananchi kuhusu hali halisi ya matumizi ya P2 nchini wakihusianisha faida na hasara za vidonge hivyo.

Mtaalamu wa afya ya uzazi kwa vijana, Waziri Njau alisema P2 zinazuia ujauzito pekee ndani ya saa 72, lakini si kinga ya kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi wala magonjwa mengine ya zinaa pamoja na saratani ya mlango wa shingo ya kizazi.

Alisema tatizo lililopo awali vijana wengi walitumia mipira ya kiume ‘kondomu’ kukwepa mimba, lakini kwa sasa wanaona P2 ndiyo mkombozi wakisahau madhara mengine ya kifya.

“Tunashuhudia leo matumizi ya kondomu yakishuka na matumizi ya P2 yakipanda na madhara ndivyo yatakavyoongezeka. Kondomu zilizuia madhara manne ikiwemo ujauzito, magonjwa ya zinaa, VVU na saratani ya shingo ya kizazi,” alisema Njau.

Alisema chanzo cha tatizo vijana wengi kutokuwa na hofu kunatokana na kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu matumizi ya vidonge hivyo ikiwa pia vinatakiwa kutumiwa baada ya ushauri wa mtaalamu wa afya.

“Hawana taarifa sahihi. Wanaona P2 ni salama, lakini wengi hawajui inatakiwa kunywewa ikiwa ni siku za hatari ambazo ujauzito unaweza kutungwa, ni mara moja kwa wiki lakini anapomeza zaidi ya mara tatu zitamsababishia mvurugo wa homoni,” alisema.

Njau alisema vijana wengi wanatumia kama njia ya uzazi wa mpango, jambo ambalo si sahihi. Hata hivyo, aliongeza kuwa matumizi hayo hayajaanza siku za hivi karibuni, kwani vijana wengi wamekuwa wakizifahamu P2 kwa muda mrefu.

“Kilichotokea si kipya, leo tunashangaa wamejuaje ukweli walikuwa wanaijua kabla ya matamko hayajatolewa,” alisema.

Hata hivyo, kitaalamu imeelezwa kuwa ndani ya mwaka mmoja, mwanamke hapaswi kumeza P2 zaidi ya mara tatu, kwani kwa kufanya vinginevyo kunaweza kutengeneza madhara mengine.

Mtaalamu wa afya ya uzazi kwa vijana na Mkuu wa Programu kutoka Youth Choice For Change (YCC), Godlove Isdory naye aliunga mkono hoja hiyo na kusema kitaalamu hushauriwa katika kipindi cha ndani ya miezi 12 mwanamke angalau ameze mara tatu.

“Hii ni kwa sababu dawa hizi zina vichocheo vikali kutoka ufananisho wake na vina nguvu ukilinganisha na vidonge vingine. Inasadikika vidonge hivi vya P2 ambavyo viko viwili ni sawa na vidonge 60 ya vidonge vya majira,” alisema.

Isdory alisema matumizi ya P2 yanahusianishwa na ongezeko la maambukizi VVU, hasa kwa vijana na hususani wa kike kwa kuwa mtumiaji hajikinga na mimba pekee, hivyo kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Ukimwi kwa urahisi.

Alisema VVU huathiri malengo ya vijana wengi hasa mtoto wa kike wenye umri kati ya miaka 14 hadi 24 wengine hushindwa kumaliza masomo, kutengwa na jamii na wengine huwasababishia vifo.

Hata hivyo, alisema hali hiyo pia itachangia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwani kundi rika linaloshambulia matumizi hayo kwa sasa ni kinamama wa baadae. “Unapozungumzia P2 unazungumzia vidonge vya uzazi vya kuzuia mimba kwa hiyo anayeshauriwa kutumia ni yule ambaye imetokea kweli bahati mbaya amekutana na mwenzake bila kujua kwamba ni kipindi cha hatari. Pia aliyebakwa au vyovyote na si yawe matumizi ya mara kwa mara,” alisema daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Living Colman.

Dk Colman alisema matumizi ya mara kwa mara ni kufanya mlundikano wa uzazi wa mpango katika mfumo wa kizazi ambao una madhara baadaye.

“Anayekusudia na kutumia mara kwa mara, ina maana kwamba anajiwekea homoni nyingi mwilini ambazo baadaye zinaweza kuvuruga mfumo wa uzazi na pengine akashindwa kupata mtoto,” alionya Dk Colman.


Usahihi wa matumizi

P2 ni dawa ya kuzuia mimba zisizotarajiwa hasa kwa wale waliobakwa, ikiwa kinga ilipasuka na kwa waliokosea hesabu za siku zao za hedhi, ili kuepuka kutoa mimba au kuzaa watoto wasiowatarajia.

Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba alisema vidonge hivyo vina majina mengi sokoni kutokana na kuwepo kwa chapa tofauti na zina uwezo wa kuzuia mimba ikiwa zitatumiwa ndani ya saa 72 tangu kufanyika tendo.

“Ukitumia ndani ya saa 24 inafanya kazi kwa nguvu kubwa na ukitumia saa 48 inapungua nguvu, lakini bado inasaidia.

“Ndani yake kuna kiambata hai ambacho ni homoni iliyopo kwenye vidonge au dawa nyingi za uzazi wa mpango ni zilezile, ila hizi zenyewe zinalengwa zitumike kuzuia mimba baada ya tendo ndani ya saa 72, mwanamke yeyote ambaye hahitaji kupata mimba,” alisema.

Alisema dawa hizo licha ya kuhusianishwa na wanafunzi, lakini hata wanandoa wengi wanazitumia, lakini bado zipo kwenye kundi la dawa ambazo lazima upate cheti cha daktari kuzinunua.

Hata hivyo, alitahadharisha kuwa dawa hiyo ina homoni na inapotumiwa hufanya mabadiliko ya homoni.

“Mimba ili itengenezwe mayai yanatakiwa yakutane na ule muunganiko wa mayai unasafrishwa kwenda katika mji wa mimba na kupandikizwa kwenye ukuta wa mimba na kuna homoni inaimarisha ukuta na mimba inakua pale mpaka mtoto anakua.

“Sasa hii dawa inakwenda kusababisha imbalance ya zile homoni haiwezekani kupandikiza mimba kwenye ule ukuta ndiyo maana inasababisha homoni imbalanece inayokuwa na manufaa wakati ule sasa ukiitumia mara kwa mara homoni zinavurugika kabisa inaanza kuleta shida mwilini.”

“Wengine wanapata shida katika mzunguko wao wa hedhi au mzunguko wa damu wanaweza kupata risk (hatari) ya kupata baadhi ya saratani katika njia ya uzazi, matiti na kwingineko bado tafiti si za kutosha bado tunahitaji tafiti za kutosha,” alisema.


Nini Kifanyike?

Mnyemba alisema bado kunahitajika tafiti za kutosha katika matumizi ya P2 nchini.

“Katika hili eneo hakuna tafiti za kutosha, inawezekana na mawazo ya watu na kama kuna tafiti zimefanyika ni chache.

“Tunahitaji tafiti za kutosha nini kimesababishwa na matumizi ya P2? Kama watafiti tunahitaji kuwa na taarifa za kutosha na bado haiondoi ukweli kwamba ukiiamini sana unajiweka katika hatari ya kupata magonjwa mengine, ni vema hizi njia zikatumika zote si mimba tu, kuna magonjwa ya zinaa.

“Kama matumizi yameongezeka ufanyike utafiti je matumizi ya P2 ni miongoni mwa chanzo cha kuongezeka kwa maambukizi haya kwa vijana?”Alipendekeza Mnyemba.

Isdory kutoka YCC alipendekeza itolewe elimu na taarifa sahihi kwa vijana hasa mabinti juu ya matumizi sahihi ya P2 na kuhamasisha utumiaji wa kondomu kwa kuwa ndiyo yenye asilimia kubwa ya kukinga vijana dhidi ya VVU au kutoanza uhusiano wa kimapenzi mpaka muda sahihi utakapofika, ili kuokoa kizazi cha sasa na baadaye.

“Kuwekwe mifumo sahihi au kutoa elimu ya kutosha kwenye maduka ya dawa (Pharmancy) ziweze kutoa elimu kwa vijana hawa na kuacha kutanguliza maslahi ya manunuzi na kusababisha kuangamiza maisha ya mabinti pia wadau tuongeze nguvu katika kushirikiana na Serikali kupunguza ongezeko hili la matumizi ya P2,” alisema Isdory.

Waziri Njau alisema nyakati za sasa stadi za maisha zinatakiwa zitolewe kwa vijana, kwani ndilo rika linalotafuta taarifa.

“Wao wanajua kuna mpaka dawa za kutolea mimba nyingi tu wanazijua, leo tunavyozungumza wanafundishwa madhara yake ni kwamba elimu katika ngazi za vijana imekuwa chini na tayari P2 siyo suala jipya limekuwepo na wamekuwa wakitumia. Madhara sasa wengi wanaambukizwa VVU kama wasipoelimishwa,” alisema Njau.


Kauli ya Waziri

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali inatamani upatikanaji wa dawa hizo usiwe na changamoto kwa kila mwenye uhitaji aliyepata dharura.

Alisema wanatambua kuna matumizi yasiyo sahihi ya hizo dawa hasa kwa wanafunzi ambao kwa sasa inaonekana wanaogopa zaidi mimba kuliko Ukimwi huku akionya kwamba matumizi holela yanaweza kusababisha madhara kiafya kwa wasichana na wanawake. Hata hivyo, aliahidi kwamba Serikali inaliangalia suala hilo kwa mapana yake wakiendelea na mjadala na tayari kuna hatua za haraka wanazichukua.

“Hatua ya haraka tutakazochukua ni kuongeza kasi ya utoaji elimu ya juu ya madhara ya matumizi holela ya dawa hizi.

“Nimeshawaelekeza timu yangu kulitekeleza hili haraka, wazazi na walezi tusione aibu kuwaeleza mabinti zetu madhara ya ngono za mapema na kuepuka ngono zisizo salama, kama msichana unaona haupo tayari kuzaa, basi unashauriwa kutumia njia za uzazi wa mpango na siyo P2,” alisema Waziri Ummy.