Zitto, Lissu wazungumzia ukaribu wao kuelekea 2020

Wednesday September 11 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Viongozi  wenye ushawishi katika siasa za upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu na Zitto Kabwe wamekana kuanzisha ushirikiano wenye maslahi ya kuongeza nguvu kuelekea katika Uchaguzi Mkuu 2020.

Jana Jumanne Septemba 10,2019 wawili hao kupitia matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW walisema ushirikiano unaotambuliwa kisheria Tanzania ni kati ya vyama na si wanasiasa.

Walisema ukaribu wao ni sehemu ya chachu katika juhudi za kuunganisha nguvu ya pamoja kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT Wazalendo hivi karibuni alikwenda nchini Ubelgiji kumtembelea Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema anayeendelea na matibabu nchini humo.

Katika mahojiano na DW, Lissu alisema ukaribu wao kama wanasiasa wamekuwa wakikutana na kujadili masuala ya namna ya kujenga mapambano ya kujenga Tanzania mpya ya kidemokrasia na inayojali haki za binadamu.

Alisema Tanzania haijawahi kuwa na mgombea binafsi, “kwa hiyo huwezi kuzungumzia ushirikiano wa kisiasa kati ya wanasiasa wawili, tunazungumza ushirikiano wa vyama na mimi siyo msemaji wa Chadema. Nafikiria hata kwa ACT  itakuwa  hivyo.”

Advertisement

Kuhusu ushirikiano unaoendelea kwa sasa Lissu alisema ukaribu wao umejengwa na misingi ya uhusiano wa muda mrefu katika siasa tangu wakiwa pamoja Chadema kabla ya Zitto kuhamia ACT Wazalendo.

SOMA ZAIDI

Kwa upande wake, Zitto alisema chama hicho kimemkabidhi mamlaka ya kuimarisha mahusiano ya upinzani kuelekea 2020.

“Juhudi hizo ni kwa vyama na watu mbalimbali katika vyama ili kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na utawala wa CCM tukiwa pamoja.”

“Kwa hiyo mahusiano, mazungumzo yanayoendelea kwa sasa yanalenga kujenga ushirikiano wa vyama na siyo ushirikiano wa mtu binafsi na mahusiano ya aina hii yanakwenda kwa utaratibu wa vyama na kwa mujibu wa sheria ya vyama,” alisema Zitto.

Zitto alisema hakuna ubaguzi katika juhudi za kujenga ushirikiano huo, akitolea mfano wa kumuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe baada ya kutuhumiwa kujihusisha na mtandao wa dawa za kulevya.

SOMA ZAIDI

Advertisement