Kilichojiri kesi ya Mbowe, wenzake hiki hapa

Thursday March 14 2019

Viongozi wa Chadema wakiwa katika kizimba ndani

Viongozi wa Chadema wakiwa katika kizimba ndani ya chumba cha mahakama ya Hakikmu Mkazi kisutu jijini Dar es Salaam.Picha na Said Khamis 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga  siku mbili mfululizo, kusikiliza ushahidi katika kesi ya kufanya mikusanyiko isiyo halali, inayowakabili vigogo tisa wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.

Pia, kesi hiyo kwa sasa itasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya hakimu aliyekuwa anasikiliza shauri hilo, Wilbard Mashauri kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Machi 14, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH).

Hakimu Simba, amesema kutokana na kesi hiyo kuwa ya muda mrefu, itabidi isikilizwe kwa siku mbili mfululizo, kuanzia Machi 28 hadi 29, 2019.

Mbowe na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo ya kufanya mikusanyiko yenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki katika Mahakama hiyo.

Awali, Wakili wa Serikali Wankyo Simon akisaidiwa na Patrick Mwita, amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupanga tarehe kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Advertisement

Baada ya Simon kueleza hiyo, Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao.

"Kesi hii ilikuwa kwa Hakimu Mashauri ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na nilivyolipitia jalada hili nimeona lina vitu vingi, hivyo itabidi washtakiwa wasomewe upya maelezo yao ya awali," amesema Hakimu Simba.

Hakimu Simba baada ya kutoa agizo hilo, Simon aliwasomea maelezo hayo washtakiwa hao ambao walikana mashtaka na kukubali majina yao.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 28 na 29, 2019 kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa ushahidi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba  112/2018 ni Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Wengine ni Naibu Katibu mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni Kinondoni ambako wanadaiwa kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.

Katika mashtaka hayo, 13 yapo ya  kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki na  kushawishi wananchi wa Kinondoni kutenda kosa la jinai kwa kubeba silaha.

Advertisement